Abdulkarim na Mariam walikutana shuleni mnamo Novemba mwaka jana. Abdulkarim aliamua kumuelezea Mariam kuhusu hisia zake baada ya urafiki wao kufikia miezi sita. Mariam hakumtarajia Abdulkarim kuchukua hatua hiyo, kwa hivyo alishikwa na bumbuwazi.
Abdulkarim akawa wa tofauti kwake kwa sababu Mariam hakumpa jibu la moja kwa moja. Siku moja, Mariam aliamua kumuomba Abdulkarim simu yake lakini, aliondoka nayo kwa siku mbili moja kwa moja bila kumrudishia. Alipokea simu zake zote, alipokuwa amemaliza kuifanyia uchunguzi, akairudisha. Mariam alimuona Abdulkarim muaminifu baada ya kuichunguza ile simu yake.
Mariam kisha akamwambia Abdulkarim ikiwa kweli anataka kuwa na yeye basi aende nyumbani na kumuomba kwa mkono wake katika ndoa. Abdulkarim alimthibitishia Mariam kuwa ana mapenzi ya kweli kwake na akatii ombi lake. Familia zote mbili zilifurahi kuona watoto wao wakichukua hatua mpya katika maisha yao.
