Mwanariadha Alphonce Simbu

Atoboa siri ya ushindi wake…. Wingi wa wenzetu unawabeba!

Wawakilishi wa Tanzania katika mbio za 14 za Standard Chartered Mumbai Marathon Alphonce Simbu na mwanadada Magdalena Krispin, wamewasili nchini huku mshindi wa mbio hizo Alphonce Simbu akitoboa siri nzito kuhusu ushindi wake ambapo alichukua nafasi ya kwanza akimtimulia vumbi mpinzani wake wa karibu Mkenya Joshua Kipkorir katika kundi la wakimbiaji wa nje. Mtanzania huyo aliongoza huku akifuatiwa na Wakenya 7 and Waethiopia 2 katika 10 bora.

Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, Simbu alilakiwa na kocha wake Francis John na Afisa muandamizi kutoka Multichoice Tanzania Johnson Mshana, mwakilishi wa Chama cha Riadha Tanzania Tulo Chambo. Pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Simbu alianza kwa kutoa shukrani kubwa kwa Watanzania wote ambao wamekuwa wakimuombea na kumtakia kila la heri. Aliipongeza kipekee kampuni ya Multichoice Tanzania kwa kukubali kumdhamini kwa muda wa mwaka mzima kitendo ambacho kimempa muda mrefu wa kufanya mazoezi na hivyo kuweza kushinda mbio hizo.

“Kwa kweli nimefurahi sana kwa ushindi huu na siri kubwa ya ushindi wangu ni kujituma, mafunzo na mazoezi” alisema Simbu na kuongeza, “Baada ya kupata udhamini kutoka Multichoice Tanzania, niliweza kutulia kwani sasa kazi yangu ilibaki moja tu, mazoezi, na kwakweli mwalimu wangu amefanya kazi ya ziada ya kunifundisha na kuniongoza pamoja na kusimamia kila kitu ikiwemo kufanya mawasiliano na waandaaji wa mashindani niliyoshiriki.”

Mkuu wa mawasiliano wa Multichoice Tanzania Johnson Mshana ambaye alikuwepo uwanjani hapo kumpokea Simbu, amesema Multichoice Tanzania imejizatiti kuinua na kuimarisha sekta ya michezo na burudani hapa nchini ikiwemo kuongeza chanel nyingi zenye maudhui ya kitanzania katika sanaa, burudani na michezo na pia katika kushiriki moja kwa moja kama ilivyofanya kumdhamini Simbu.

 “Bila kuvipalilia vipaji tulivyonavyo, itakuwa vigumu sana kufikia malengo, ndiyo sababu sisi Multichoice Tanzania tumeamua kutia nguvu katika kukuza vipaji vya watanzani” alisema Mshana na kuahidi kuwa wataendelea kumuunga mkono simbu ili wafanikiwe katika lengo la kushinda katika michuano ijayo ya kimataifa.

Mwalimu wa mafunzo wa Mkimbiaji huyo Francis, alimtaja Simbu kuwa ni mwanariadha mwenye kipaji kikubwa na nidhamu ya hali ya juu, mbali na jitihada kubwa anazofanya kila siku kuhakikisha kuwa anatimiza ndoto zake.

“Alphonse ni kijana mwenye bidii, juhudi na maarifa, na zaid ya yote ni kipaji chake na nidhamu yake ya hali ya juu” alisema Francis na kuongeza kuwa  sisi multichoice tumeTulichukua jukumu la kumdhamini simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote. Alisema Mshana na kuongeza “dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani”

Katika mbio hizo, aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa 2:09:28 muda ambao ni mzuri sana kwa mbio za aina hiyo. Mwezi April mwaka huu, Alphonce anatarajiwa kushiriki mashindano mengine makubwa Ulimwenguni ya London Marathon